• Home
  • /Uncategorized
  • /MAONESHO YA NANE NANE – KANDA YA KATI DODOMA. KESHO KUFIKIA SIKU YA KILELE CHA MAONESHO

MAONESHO YA NANE NANE – KANDA YA KATI DODOMA. KESHO KUFIKIA SIKU YA KILELE CHA MAONESHO

Kesho, tarehe nane (08) mwezi wa nane (08) wananchi wote wa Tanzania watakuwa wanasheherekea kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima – NaneNane. Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2017 ni ‘ZALISHA KWA TIJA MAZAO NA BIASHARA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI ILI KUFIKIA UCHUMI WA KATI’. Wananchi mnakaribishwa kutembelea banda la Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), uwanja wa maonesho ya kilimo – NaneNane, Kanda ya kati Dodoma.

Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi – TAMISEMI, na Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) wamejumuika na wadau wengine katika kutoa elimu juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, kadhalika na jinsi gani mabadiliko hayo yanachangia  uchumi wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Maonesho haya yanafanyika kitaifa mkoa wa Lindi na kwa Kanda ya kati kitaifa yanafanyika Dodoma.

Mkuu wa Mkoa, Mh. Dr. Rehema J. Nchimbi alifungua rasmi maonesho ya kanda ya kati Dodoma  siku ya tarehe tatu (3). Katika hotuba yake alisisitiza kuwa; wadau wote walio hudhuria ama walio na banda hapa uwanja wa nanenane wanatakiwa kutoa elimu itakayowawezesha wananchi kuelewa mikakati endelevu ya kukuza uchumi. Aliendelea kusisitiza kuwa, “kwa taasisi na mashirika na wajasiriamali mliopo leo, na mliokuwepo miaka ya nyuma, mtoe elimu itakayo onyesha hatua mliyopiga toka mwaka jana na miaka ya nyuma, na mikakati mliyotumia katika kukuza uchumi. Nina amini kuna mafanikio mazuri na ndio maana mmeweza kuja tena kwenye maonyesho ya mwaka huu wa 2017”. Alimalizia kwa kusema, “elimu ianzie kwa mama lishe mpaka kwenye halmashauri na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali. Wananchi, mkitembelea mabanda dadisi njia mbadala ambazo wenzetu wanazitumia katika kupiga hatua kwenye kukuza uchumi”.

Kadhalika maonesho haya ya kanda ya kati Dodoma yametembelewa na viongozi mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya, Bi. Christina S. Mndeme, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Jabir M. Shekimweri, Meya wa Manispaa ya Dodoma – Prof. Davis Mwamfupe na Spika Mstaafu Mh. Anna S. Makinda.

Kwenye upande wa mradi wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, kumekuwa na maelezo mengi na jumbe mbali mbali zilizotolewa na wadau wa mradi. Hii ikiwa ni pamoja na kusisitiza kuwa; “Taarifa ni muhimu sana kwa kila mwananchi, wananchi wanatakiwa kuwa na shauku ya kutaka kujua jinsi gani wanaweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi huku wakihakikisha wanakuwa na njia mbadala ya kukuza uchumi kuanzia ngazi ya familia, hii ikiwa ni pamoja na kuwa na uhakika wa chakula na malazi. Mradi huu upo hapa uwanja wa nanenane Dodoma kwa lengo kubwa la kuhakikisha kila mwananchi anapata taarifa juu ya mradi na kujifunza jinsi gani wananchi wa Monduli, Longido na Ngorongoro wameweza kubuni miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi” alisema Bi. Sophia Masuka – Mratibu wa Mawasiliano, Jumuiko la maliasili Tanzania.

Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ni wa miaka mitano (5) unaolenga kuwekeza kwenye miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika wilaya kumi na tano (15) Tanzania bara; Bahi, Iramba, Kilwa, Kiteto, Kondoa, Longido, Manyoni, Mbulu, Mpwapwa, Monduli, Ngorongoro, Pangani, Same, Siha na Simanjiro.

Mradi huu utatekelezwa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza (2016-2018) itakuwa chini ya uratibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira  na Maendeleo (IIED), na itahusisha wilaya tatu za majaribio (Monduli, Longido na Ngorongoro), na awamu ya pili  (2018 – 2021) utakuwa chini ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI ) na itahusisha wilaya kumi na mbili (12) zilizobaki.

Mradi unafadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKAID), kwa msaada wa kiufundi kutoka IIED na Umoja wa Mataifa “Capital Development Fund” ( UNCDF LoCAL).

Leave a Reply